TUMEHAMA

tumehamia www.johnkitime.co.tz karibu

Monday, May 4, 2015

FRANKLIN BOUKAKA MWANAMUZIKI ALIYEUWAWA KWA SABABU YA SIASAFRANKLIN  alikuwa mtoto wa mwanamuziki Aubin Boukaka wa kundi la "The Gaiety ", na mkewe Yvonne Ntsatouabaka aliyekuwa MC maarufu  kwenye misiba na pia alikuwa mwanamuziki muimbaji.  François Boukaka aliyekuja julikana kama Franklin alizaliwa tarehe  10 Oktoba, 1940. Yeye ndie alikuwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanane wavulana watatu na wasichana watano. Elimu yake yote aliipata katika shule mbalimbali nchini kwake Congo Brazzaville. Franklin  alianza mambo ya muziki 1955 katika kundi lililojiita Sexy Jazz lililoongozwa na Miguel Samba, baadae akaanzisha kundi la Negro Band. Hatimae katika safari yake ya muziki akaungana na wakali wengine kama  Edo Clary Lutula, Jeannot Bombenga, Tabu Ley , Mutshipile "Casino", André Kambite " Damoiseau ",  Papa Bouanga, Charles Kibongue katika lile kundi maarufu la African Jazz, sauti ya Franklin imo katika nyimbo kama  Mwana mawa , Catalina cha cha na Marie José zilizotungwa na Tabu Ley. Mwaka 1959 kundi la African Jazz lilimeguka baada ya wanamuziki wengine walipohamia Brussels wakifuatana na wanasiasa wa Kongo kwenye mazungumzo ya awali ya uhuru wa Kongo. Wanamuziki wote waliobaki akiwemo Jeannot Bombenga,  kasoro Tabu Ley wakajiunga na kuanzisha kundi jingine lililotingisha Africa lililoitwa Vox Africa, Franklin Boukaka na Jeannot Bombenga wakiimba. Baada ya hapo Franklin akaaliacha kundi hili na kurudi kwao Brazzaville ambako  1962 akawa mmoja wa wanamuziki wa Cercul Jazz, band iliyoanza miaka ya 50 ikiwa chini ya chama cha vijana kilichokuwa kikipata ufadhili wa serikali ya Ufaransa, chama hicho kiliitwa Cercule Culturel de Bacongo.  Hatimae Boukaka alikuja kuwa kiongozi wa chama hiki na kikawa na umaarufu wa mkubwa. Wimbo wa bendi hiyo "Pont Sur le Congo" (Daraja juu ya Mto Congo), wimbo ambao ulikuwa una hamasisha kuunganika kwa Congo Kinshasa na  Kongo Brazzaville baada ya nchi hizo kupata uhuru. Wimbo uliopata umaarufu kuliko nyimbo zote za bendi hiyo. Baadaye Franklin akiwa na gitaa lake kavu akaanzisha kikundi ambacho kilikuwa na wapiga marimba wawili akaweza kufanya ziara kadhaa hata nje ya nchi yake na kundi hili. Mwaka 1970 ndipo Boukaka  alipo rekodi nyimbo 12 zilizopangwa vyombo na Manu Dibango na hapo ndipo nyimbo Nakoki na Le Bucheron zilipopatikana. Baada ya hapo Franklin alijiunga na wenzie waliotaka kuipindua serikali ya Congo Brazzaville wakati huo ikiwa chini ya Rais Marien Ngouabi(aliyetuletea suti za Ngwabi). Jaribio hilo lililofanyika tarehe 22 February 1972 lilishindwa na siku chache baadae kifo cha Boukaka kilitangazwa.

Thursday, April 23, 2015

MWANAMUZIKI MKONGWE MUTOMBO LUFUNGULA AUDAX HATUNAE TENA

AUDAX(kushoto) akiwa na Kasongo Mpinda
Mwanamuziki muimbaji na mtunzi mashuhuri wa bendi ya Maquis Original Mutombo Lufungula Audax, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, huko Kimara Michungwani. Mwili wake umepelekwa kuhifadhiwa Mwananyamala Hospitali. Audax alikuwa ndie mmoja wa wanamuziki asili wa kundi la Maquis Du Zaire. Kundi la Maquis lilianza katika mji wa Kamina, jimbo la Shaba, huko Kongo. Awali kundi lilianza kwa kuitwa Super Teo, kisha kubadili jina na kuitwa Rocken, ......INAENDELEA

Tuesday, April 21, 2015

MWANAMUZIKI WA SIKU NYINGI PAUL GAMA AFARIKI DUNIA

KWA MASIKITIKO MAKUBWA TUMETAARIFIWA KUWA MWANAMUZIKI WA ZAMANI PAUL GAMA AMEFARIKI DUNIA HUKO DODOMA TAREHE 16.4.2015 MUDA WA SAA NNE ASUBUHI. NARUDIA MAKALA HII YA HISTORIA YA PAUL GAMA KADRI ALIVYOTUELEZA MWENYEWE

Paul Daniel Gama
Paul Daniel Gama alizaliwa Barabara ya 11 Dodoma (1947). Baba yake alikuwa ni mwanajeshi wa KAR mwenye asili ya Songea na mama yake alikuwa na asili ya Usangu alikuwa anafanya kazi  katika 
Spokes Mashiyane na filimbi yake
hospitali ya Mirembe ambayo wakati huo ilikuwa ni hospitali kubwa ya majeruhi wa vita ya pili ya dunia. Aliingia shule na alipofika darasa la nne alijikuta akiwa na kipaji kukubwa cha kupiga filimbi, wakati huo wapiga filimbi walipenda sana kumuiga mpiga filimbi maarufu kutoka Africa ya Kusini Spokes Mashiyane. Akiwa na wenzie walianzisha kikundi ambacho kilikuwa na maskani eneo la Mji Mpya pale Dodoma. Vijana hao pia walikuwa wakiiga  nyimbo za wanamuziki maarufu wa wakati huo, kama Salum Abdallah na  Cuban Marimba, pia Salum Zahor na Kiko Kids. Katika kufanya fani yao hiyo kama kitu cha kujipa burudani waliligusa sikio la  aliyekuwa mwalimu wa Elimu ya Watu Wazima katika Community Center ya pale Dodoma. Mwalimu huyu aliwasaidia kuwaazimia amplifaya moja kutoka kwenye bendi nyingine ilikuweko Dodoma wakati huo, The Jolly Sextet Band. Band iliyokuwa ikimilikiwa na Mkenya mmoja ambaye alifika Dodoma kama mfanya kazi wa East African Postal and Telecommunication Services, huyu bwana alikuja na vyombo vingi akaanzisha bendi ambayo mmoja wa wapigaji wake alikuwa Mzee Mnenge ambaye hatimaye alitua NUTA Jazz Band.
Bongos
Hiki kikundi cha Gama na wenzie kilikuwa katika mfumo wa Jazz Band za zamani ambapo walikuwa na ngoma na filimbi tu,ikisindikizwa na kuimba, lakini waliweza kukonga nyoyo hata za wanamuziki wengine, na Gama akawa anasakwa na bendi kubwa iliyokuweko wakati ule Central Jazz band. Alipomaliza darasa la saba tu ndugu yake aliyeitwa Titus Olaf Gama alimshawishi aingie Central Jazz lakini hakuwa tena mpiga filimbi bali mpiga Bongos, fani aliyoiweza sana hata  kuipenda na hasa baada ya kuwaona wanamuziki wa NUTA akiwemo Muhidin Gurumo  ambaye wakati huo alikuwa akipiga Bongos na kuimba. Bongos no ngoma ndogo zilizokuwa muhimu katika kundi wakati huo ambapo hakukuweko na drums wala tumba. Taratibu akaanza kupata hamu ya kupiga bass, wanamuziki wenzie walimkatisha sana tamaa kwa kuambiwa kuwa vidole vyake vilifaa sana kwa kupiga bongos na si kupiga gitaa.

Katika jitihada zake za kujifunza gitaa la bezi alikuwa kila mara akiwahi mazoezi na kujaribu kujifunza gitaa la bezi. Hilo lilikuwa gumu mpaka pale bendi  ya Lake Jazz Band ilipotembelea Dodoma. Bendi hiyo wakati huo ikiwa na wanamuziki kama Shem Karenga  akiwa anapiga gitaa la bezi, Mzee alum ambaye alikuwa na ulemavu wa macho, mwanzo alikuwa akipiga gitaa la solo na baadae akahamia kupiga gitaa la rhythm wakati gitaa solo lilikuja kupigwa na jamaa aliyeitwa Kally. Kutokana na simulizi ni wazi kuwa wanamuziki wa kutoka Burundi walikuwa wengi sana nchini wakati huo. Pia katika bendi hiyo alikuweko Mzee Juma Kitambi, mtunzi wa wimbo maarufu wa Rangi ya Chungwa.
Gama alichukua nafasi hii kumfuata Mzee Salum ili aweze kumfundisha gitaa. Kwa kuwa wanamuziki wengine walikuwa wakitoka kwenda kutembea Mzee Salum alibaki nyumbani na hivyo Gama alichukua nafasi hiyo kumnunulia sigara Mzee Salum ana kumsihi amfundishe gitaa nae alifanya hivyo na Gama akatokea kuwa mpiga bezi mahiri.
Katika kipindi hiki akatokea mfanya biashara Mohamed Omar Badwel, huyu alikuwa na gereji na studio ya kupiga picha, aliweza kwenda Mombasa na kurudi na seti ya vyombo na kuanzisha Dodoma Jazz Band. Gama akahama Central Jazz Band na kujiunga na wanamuziki wengine walioanzisha Dodoma Jazz. Band ilianza ikiwa na mpiga solo Hassan Mursali mwanamuziki mweny asili ya Malawi, siku hizo ikiitwa Nyasaland alikuwa ndie mpiga solo, lakini aliwaacha baadae na kujiunga na NUTA Jazz Band, upigaji wake wa solo unaweza kuusikia katika kusikiliza kibao kimoja maarufu cha NUTA, kilichoitwa Dunia Njema Kukaa Wawili.
Hasan alikuwa mtu wa kuhama hama hatimae alipoteza uwezo wa kusikia jambo ambalo lilihusishwa na kuhamham kwake kwani ushirikina ulitawala sana wakati huo, kama maelezo yanayofuata yanavyoonyesha. Dodoma Jazz ilikuwa pia inafanya ziara katika sehemu nyingi , kama vile Iringa, Mbeya ,Tabora, Dar es Salaam na kadhalika, lakini safari moja ya kwenda Kilosa ilifanyika ikiwa na lengo la kumfuata Abel Barthazal aliyekuwa akipiga katika bendi ya Kilosa Jazz. Bendi  ilipokelewa vizuri na wakafanya maonyesho yao Kilosa na hatimae kuondoka na Abel. Siku chache baade wakati huo Mzee  Mohamed Omar, mwenye bendi alikuwa kasha mnunulia suti kadhaa Abel, ukaja ugeni toka Kilosa wakiwa na barua yenye maelezo kuwa ikiwa Abel Hatarudi Kilosa, mmoja wa wanamuziki wa Dodoma Jazz atafariki, na barua hii ililetwa kwa mkono na mjumbe ambae alisisitiza wakishaisoma mbele yake ndio anaondoka. Abel alirudishwa Kilosa mara moja.
Baada ya hapo aliyekuwa meneja wa bendi Ramadhan Waziri alitumwa Burundi kwenda kutafuta wapigaji, siku alipokuwa anarudi na wapigaji wapya akakutana kwenye treni na Rashid Hanzuruni, mpiga solo mahiri sana ambaye upigaji wake husikika katika wimbo  Napenda nipate lau nafasi
Hanzuruni alikuwa kaiacha Tabora Jazz baada ya  kutokea ugomvi mkubwa ambapo alipoteza meno kadhaa, hivyo alikuwa kwenye hilo treni akielekea Dar es Salaam kumfuata mpigaji mwenzie Samba ambae alikuwa NUTA Jazz. Ramadhani aliweza kumshawishi hanzuruni akabaki Dodoma Jazz ambako alikaa kwa muda na hatimae akaja kuchukuliwa na Sama ili aingie NUTA Jazz, ndoto hiyo haikufanikiwa kwana NUTA alikuweko mpigaji mahiri  Hamisi Franco, hii ndiyo ilipelekea Hanzuruni kwenda Western Jazz BandTuesday, March 24, 2015

HAKIMILIKI ZA MARIJANI RAJABU

Marijani Rajabu alizaliwa tarehe 03 March, 1955 katika eneo la Kariakoo Dar es Salaam. Siku ya tarehe 23 March 1995 Marijani Rajabu- Jabali la Muziki, Doza aliaga dunia. Tunatimiza miaa 20 toka tulipoonana mara ya mwisho na mwamba huu. Nakumbuka nilipokutana nae mara ya mwisho, alikuwa kiuza kanda za nyimbo zake katika kaduka kadogo alikofungua nyumbani kwake...endelea huku

Friday, January 16, 2015

IMETIMIA MIAKA 36 TOKA KIFO CHA MBARAKA MWINSHEHE, MUZIKI WAKE BADO UKO HEWANI

Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alizaliwa mjini Morogoro Juni 27, 1944. Siku ya Januari 12, 1979 ulimwengu wa muziki Tanzania ulitikiska kwa simanzi baada ya kusikika kifo cha mwanamuziki huyo, mpiga gitaa muimbaji, mtunzi na kiongozi wa bendi wa miaka mingi na ambaye bendi yake ilikuwa imepiga karibu kila wilaya ya nchi hii. Taarifa ziliingia jioni ya siku ile kupitia redio ya Taifa kuwa nguli huyu alifia katika hospitali katika jiji la Mombasa nchini Kenya muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya gari...........ENDELEA HUKU

Tuesday, December 16, 2014

HATIMAE SHEM IBRAHIM KARENGA AZIKWA

HATIMAE  mwanamuziki mkongwe mpiga gitaa muimbaji na mtunzi mahiri Shem Ibrahim Karenga amezikwa katika makaburi  ya Kisutu jioni ya leo. Shughuli hiyo ilianza kwa utata baada ya kuwa makaburini hapo kulikuwa na misiba minne hivyo kila lilipokuja jeneza wanamuziki, ndugu na wapenzi wa muziki walijikuta wakisindikiza jeneza na..........INAENDELEA HUKU